Mchungaji Msigwa ambaye ni mshtakiwa wa saba katika kesi zote mbili amefikishwa mahakamani leo Jumatano Januari 24,2018 baada ya kuripoti kituo kikuu cha Polisi.

Katika kesi hiyo namba 6 ya mwaka 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, David Ngunyale, Wakili wa Serikali, Felix Chakla amedai kati ya Januari 5 na 14,2018  washtakiwa walipanga njama za kuharibu mali.

Pia wanadaiwa Januari 15,2018 walibomoa nyumba ya Anjelus Mbogo aliyekuwa diwani wa Mwangata aliyejiuzulu kutoka Chadema na kuhamia CCM.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema Iringa Mjini, Leonce Marto; diwani mteule wa Viti Maalumu, Rehema Mbeta na Patrick Madati.

Mchungaji Msigwa na wenzake wako nje kwa dhamana baada ya kila mmoja kusaini bondi ya Sh2 milioni.

Katika kesi ya pili, Mchungaji Msigwa na wenzake sita wanadaiwa kupanga njama ya kutenda uhalifu kinyume cha sheria.

Wakili Chakla mbele ya hakimu Ngunyale amedai Januari 17,2018  washtakiwa kwa pamoja walichoma nyumba ya Tesha aliyokuwa akiishi Muyinga.

Kwa shauri hilo namba 7 la mwaka 2018, washtakiwa wanadaiwa Januari 17,2018 waliichoma moto nyumba hiyo iliyopo kata ya Kihesa katika Manispaa ya Iringa.

Washtakiwa walikana kosa na hakimu  Ngunyale aliwaachia kwa dhamana baada ya kila mmoja kudhaminiwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh3 milioni.


Mchungaji Msigwa na wenzake katika kesi hizo wanawakilishwa na wakili wa kujitegemea Anthony Rutebuka. Hakimu Ngunyale ameahirisha kesi hizo hadi Februari 2,2018.

Post a Comment

Powered by Blogger.