Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inatarajia kuanza kutoa huduma ya upasuaji mkubwa wa magonjwa ya ini na upandikizaji wa ogani hiyo, baada ya kupeleka wataalamu saba nchini India leo kwa ajili ya mafunzo.
Matibabu hayo ya kibingwa nchini yataokoa zaidi ya Sh100 milioni ambazo Serikali ilikuwa ikizitumia kwa mgonjwa mmoja aliyepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya upandikizaji wa ini.
Novemba 21, Muhimbili ilifanya upasuaji wenye mafanikio na wa kwanza baada ya kupandikiza figo kwa mwanamke wa miaka 30 ambaye figo zake zilikuwa hazifanyi kazi.
Akizungumza na vyombo vya habari jana, mkuu wa kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema wanapeleka wataalamu hao kwa ajili ya mafunzo ya kufanya upasuaji mkubwa.
“Timu hii ya wataalamu inayoondoka kesho (leo) inajumuisha madaktari bingwa wanne wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, wauguzi wawili wanaosimamia mifumo ya hadubini na mhandisi wa vifaa tiba anayesimamia mitambo ya hadubini,” alisema Aligaesha. Alisema mafunzo hayo yatachukua muda wa miezi mitatu na wanatarajiwa kurejea nchini wiki ya kwanza ya Machi 2018.
Aligaesha alisema ni matarajio yao kwamba wataalamu hao watakaporudi wataongeza ufanisi katika kufanya uchunguzi na tiba ya magonjwa ya ini kwa kutoa mawe, kuzibua mifereji ya nyongo na kongosho iliyozibwa na uvimbe.
“Tutaweza kufanya upasuaji wa ini kuondoa uvimbe mkubwa unaoodhofisha afya na kutishia maisha ya wagonjwa. Aidha lengo kubwa ni kujenga uwezo wa ndani kwa muda mfupi utakaowezesha kufanyika kwa upandikizaji wa ini kwa wagonjwa wenye mahitaji,” alisema Aligaesha.
Mkuu wa kitengo cha Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini, Dk John Rwegasha alisema wagonjwa wenye matatizo ya ini ongezeko lao ni kubwa, hivyo ni muda muafaka kwa nchi kujikita katika matibabu hayo.
Alisema kati ya wagonjwa wanaolazwa katika kitengo cha magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, asilimia 60 wanaugua ini na hufika hospitali katika hatua za mwisho za ugonjwa.
Hata hivyo, alisema gharama za kutibu ini au upandikizaji ni zaidi ya Sh100 milioni nchini India, hivyo huduma hiyo ikianza kutolewa hapa nchini itapunguza nusu ya gharama. “Tulikuwa tunawahudumia mpaka wanapofariki, hatukuwa na morari ya kuwapeleka nje kwani kupandikiza ini si kwa hatua za mwisho, bali kwa hatua za awali za ugonjwa, hivyo tukikamilisha utaalamu huu tutawatafuta katika hatua za awali na kuzuia uharibifu wa ini zaidi kwa kuwafanyia upasuaji au kupandikiza ini,” alisema Dk Rwegasha.
Daktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa chakula, Ally Mwanga alisema baada ya kupata mafunzo wanatarajia kutoa matibabu kwa wagonjwa wengi wanaosumbuliwa na saratani ya ini na homa ya ini.
“Kwa kuwa tumepanua huduma zetu za uchunguzi, tutaanza sasa kutoa tiba kwa kumsaidia mgonjwa kutoa uvimbe au kufanya upandikizaji wa ini jingine kama ugonjwa unagundulika kwa hatua za mwanzo, miundombinu ipo kwa sasa na tuna vyumba vya upasuaji na ICU za kutosha,” alisema Dk Mwanga.
Post a Comment