Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ameishukuru serikali ya watu wa China kwa msaada wao walioutoa kwa wananchi wa Tanzania wa kuwapatia matibabu bure, akisema jambo hilo ni upendo usio elezeka.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo alipoenda kutembelea meli yenye madaktari bingwa kutoka nchi China ambayo imetia nanga katika bandari ya Dar es salaam hivi karibuni, na kutoa huduma za matibabu pamoja na vipimo bure kwa wananchi wa Jiji la Dar es salaam na maeneo jirani.

"Tunapenda kusema shukrani kwa dhati kwa serikali ya China kuamua kuituma meli na madaktari kuja Tanzania, tunafurahi kwa huduma zao, wameokoa maisha ya watanzania zaidi ya elfu 6,400, huu ni upendo wa pekee unaogusa, ndio maana leo nimeshindwa kuvumilia nimeona bora nije nishukuru, nimeguswa mno na ndugu zetu wachina, yapo mataifa mengine matajiri, yenye mali nyingi lakini hayajaguswa", amesema Rais Magufuli.

Sambamba na hayo Rais Magufuli amewakabidhi madaktari hao barua maalum kwenda kwa Rais wa nchi yao Xi Jinping pamoja na kumzawadia zawadi ya kinyago, kumshukuru kwa mchango wake na ukarimu wake alieuonyesha  kwa watanzania masikini.

Pia Rasi Magufuli amewatakia safari njema madaktari wote hao na kuwaomba kurudi tena wakati mwengine, na kuwataka kukaa kwa muda mrefu zaidi ili waweze kutoa huduma kwa watanzania wengi hata kwa wale watakaotoka mikoani.


Post a Comment

Powered by Blogger.