Jeshi la Polisi limesema limepokea agizo la Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla la kuwachukulia hatua watu wanne
ndani ya siku saba kwa madai wanashiriki katika mtandao wa ujangili, lakini
halifanyi kazi kwa shinikizo.
Msemaji wa Jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa amesema
polisi wanafanya kazi kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za Jeshi hilo.
Juzi,
Kigwangalla mbali na kutoa agizo hilo, amesema watu hao wanne pia
walipanga njama za kumuua mwanaharakati, Wayne Lotter na kwamba polisi
wakishindwa kuwakamata atawashtaki kwa Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwakalukwa amesema jukumu lao ni kukamata wanapopata
shitaka la kuwapo kwa kitu kisicho cha kawaida, kuchunguza na kupeleka kwa Mkurugenzi
wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kukamilisha taratibu nyingine.
“Kazi yetu ni kukamata, kuchunguza na kupeleka
kwa DPP kwa ajili ya taratibu nyingine,
hatufanyi kazi kwa matamko ya bungeni,” amesema na kuongeza;
“Alichokisema mheshimiwa Kigwangalla nimekisoma
kwenye vyombo vya habari akihusisha na suala la mwanaharakati aliyeuawa, sisi
hatufanyi kazi kwa kufuata vyombo vya habari vimeandika nini au limetolewa
tamko gani au kuna shinikizo gani, tunafanya kwa kufuata taratibu zilizopo.”
Post a Comment