Mghana Bernard Arthur, mshambuliaji mpya wa Azam FC amewasili asubuhi ya leo Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam tayari kuanza maisha mapya na Azam FC ndani ya Chamazi.
Arther aliyesaini miaka miwili na klabu ya Azam FC akitokea kwenye timu ya Liberty Professional ya kwao, Ghana, amewasili leo akiongozana na Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdul Mohamed ambaye alimfuata nchini humo kukamilisha usajili wake.
Akizumgumza jijini Dar es Salaam leo, Ofisa Habari wa Azam, Jafari Idd alisema kuwa, mchezaji huyo raia wa Ghana tayari ameungana na timu huku akisubiri uongozi wa klabu hiyo wakishughulikia vibali yake kwa ajili ya kuanza kazi rasmi na matajiri hao wa chamazi.
“Mchezaji wetu mpya wa Ghana, amewasili alfajiri ya leo nchini akiwa na Mtendaji mkuu wa Azam, Abdul Mohamed, tayari ameungana na timu Chamazi huku akisubiri uongozi kushughulikia vibali vyake ili aweze kuanza kazi rasmi,” alisema Jafari.
Usajili wa Arthur ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi la timu hiyo kwenye usajili huu wa dirisha dogo, anayekuja kuziba pengo la straika mwingine, Yahaya Mohammed, aliyeondoka kwa makubaliano maalumu ya pande mbili wiki chache zilizopita.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya WAFA (Ghana) na Asec Mimosa ya Ivory Coast, anaungana na washambuliaji wengine wa timu hiyo katika kukiongezea makali kikosi hicho, ambao ni Mbaraka Yusuph, Wazir Junior, Yahya Zayd, Shaaban Idd pamoja na wale waliopandishwa kutoka Azam B, Paul Peter na Andrea Simchimba.
Hadi sasa timu inajiandaa kwa ajili ya mechi yao ya kesho dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro, katika mchezo wa raundi ya 11 ya Ligi Kuu Bara utakaopigwa kuanzia majira saa moja usiku kwenye Uwanja wao wa nyumbani Azam Complex uliopo Chamazi.
Wakati huo, nyota wawili wa Azam FC, Shaaban Idd na Joseph Kimwaga, ambao ni majeruhi sasa huenda wakarejea dimbani Januari Mosi mwakani wakati timu hiyo itakapokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar.
Post a Comment