Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child Heart – SACH) ya nchini Israel wamefanikiwa kufanya upasuaji wa Moyo kwa watoto 20 wenye matatizo ya Moyo bila kufungua kifua (Catheterization).
Upasuaji huo unatumia mtambo wa Cathlab ambao umefanyika katika kambi maalum ya matibabu iliyoanza tarehe 23/11/2017 na kutarajiwa kumalizika kesho tarehe 27/11/2017. Matibabu hayo yaliyofanyika ni pamoja uzibaji wa matundu kwenye moyo na kutanua mishipa ya Moyo.
Katika kambi hii tunatarajia kufanya uchunguzi wa moyo kwa watoto 100 kati ya hao watoto 60 ambao watakuwa na matatizo makubwa watapelekwa nchini Israel kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua mwakani na watoto 40 watatibiwa hapa nchini.
Tumepanga kufanya matibabu kwa watoto 25 tunaamini hadi kambi itakapomalizika watoto wote hawa watakuwa wamepata matibabu. Watoto 20 waliopata matibabu wengine wameruhusiwa na waliobaki hali zao zinaendelea vizuri na wataruhusiwa pindi afya zao zitakapoimarika.
Tangu mwaka 2015 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilianza kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child Heart- SACH) ya nchini Israel ambapo hadi sasa jumla ya watoto 40 wamefanyiwa upasuaji wa moyo nchini Israel. Gharama za matibabu ya watoto hawa zinagharamiwa na Taasisi hii.
Tunawashukuru sana wenzetu hawa wa SACH kwa kuona umuhimu wa kutoa huduma ya matibabu bure kwa watoto wenye matatizo ya moyo. Watoto waliotibiwa wamepona na wale ambao walikuwa wanafunzi wanaendelea na masomo yao.

Post a Comment